ENEO LA 1 1.7 Taarifa za umma zinapatikana kwa urahisi kwa umma na zinatambulika kisheria Baada ya miaka mingi ya ushawishi wa vyombo vya habari na watetezi wa haki za binadamu, hatimaye Tanzania ilipitisha Sheria ya Upatikanaji wa Habari ya mwaka 2016. Kifungu cha 5(1-3) cha sheria hiyo kinasema kwamba: Kila mtu atakuwa na haki ya kupata habari ambayo iko chini ya udhibiti wa mwenye habari hizo. Mmiliki wa habari, kwa mujibu wa Kifungu cha 6 na sheria nyinginezo zozote zilizo kwenye maandishi, atatoa taarifa kwa umma au, akiombwa kufanya hivyo, kwa mtu yeyote, taarifa anazozimiliki yeye. Hakuna chochote katika Sheria hii ambacho kitakwamisha au vinginevyo kuzuia matakwa ya sheria nyingine yoyote ya mamlaka ya umma kutoa taarifa. Sheria hiyo (Kifungu cha 7-9) kinabakiza kanuni za wajibu wa kutoa taarifa, wajibu wa kutunza taarifa na wajibu wa kuandika taarifa fulani. Miongoni mwa vifungu vingine, sheria inazitaka mamlaka kuteua maafisa habari kwa ajili ya ‘kushughulikia maombi ya taarifa na kutoa usaidizi kwa mtu anayetafuta taarifa hizo’. Sheria inabainisha taratibu za kupatiwa taarifa kwenye Vifungu vya 10 na 11, ambazo ni pamoja na kutoa kipaumbele kwa watu wasiojua kusoma na kuandika na watu wenye ulemavu. Pamoja na hatua hizi chanya, washiriki walisema kwamba Sheria ya Upatikanaji wa Habari bado haijitoshelezi. Mathalan, hakuna uwajibikaji kwa wamiliki wa habari ambao hawataheshimu maombi ya habari. Walifanya ulinganisho na India ambapo sheria kama hiyo inasema kwamba afisa habari atakayeshindwa kuheshimu maombi ya habari anawajibika kama yeye. Sheria ya Tanzania pia inawapa maafisa habari au watu wanaokaimu nafasi hizo, hadi mwezi mmoja ili kujibu maombi ya habari, na hivyo kuweka kigingi kwa watu ambao wanaoweza kuhitaji habari kwa haraka kama vile wanahabari na wanasheria. Aidha, Kifungu cha 18 kinaweka mipaka kuhusu namna ambayo habari zilizotolewa zinaweza kutumiwa, na kueleza muda wa kifungo cha hadi miaka miwili jela kwa mtu atakayekutwa na hatia ya kubadilisha habari zilizopatikana kwa njia ya ombi la Uhuru wa Habari (FOI). Tangu Sheria ya Upatikanaji wa Habari ilipopitishwa, wanajopo wanasema kwamba, kwa mshangao, upatikanaji wa habari umekuwa mgumu zaidi kwa umma na kutolea mfano tafiti mbili zilizofanywa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) na Baraza la Habari Tanzania, ambazo zilionesha kwamba sheria hii haijaboresha upatikanaji wa habari. Washiriki walieleza kwamba kwa utaratibu wa kuteua maafisa habari, baadhi ya mamlaka za umma – kama vile serikali za mitaa, ambazo kiasili huwasiliana na wapiga kura, wameacha utaratibu wao wa kutumia mbao za matangazo na njia nyinginezo za mawasiliano. Kumekuwepo pia na kushuka kwa haraka kwa upatikanaji wa habari kwenye tovuti za kiofisi na mitandao mingine ambayo ilikuwepo chini ya utawala wa uwazi kabla ya mwaka 2016. Badala ya kuendeleza, washiriki waliona kwamba Sheria ya Upatikanaji wa Habari ilikuwa imeweka vikwazo kwa upatikanaji wa habari. 22 KIPIMO CHA VYOMBO VYA HABARI BARANI AFRIKA TANZANIA 2019